Aristoteli
Kutoka Wikipedia
Aristoteli (Kigiriki Αριστοτέλης aristotelēs; pia: Aristo) (* 384 KK - † 7 Machi 322 KK) alikuwa mwanafalsafa muhimu wa ustaarabu wa Ugiriki ya Kale.
Pamoja na Plato huhesabiwa kati ya wanafalsafa muhimu zaidi katika utamaduni wa magharibi. Aristoteli alikuwa mwalimu wa Aleksander Mkuu kabla huyu hajakuwa mfalme bado.
Yaliyomo |
[hariri] Maisha
Aristoteli alizaliwa kwenye rasi ya Halkidiki katika Ugiriki ya kaskazini kama mtoto wa mganga wa mfalme Amyntas wa Masedonia. Alipofikia umri wa miaka 17 au 18 alitumwa kusoma kwenye chuo ya Plato huko Athens alipokaa kwa miaka 20 mwanzoni kama mwanafunzi baadaya kama mwalimu. Baada ya kifo cha Plato mwaka 347 alisafiri akatembelea mahali mbalimbali kwenye visiwa vya Bahari ya Aegei pamoja na Asia Ndogo. Akakaa kwa mfalme Hermias wa Assos akamwoa binti yake Phytias. Mnamo 345 Hermias aliuawa na Wajemi na Aristoteli alipokea wito la kuwa mwalimu wa mfalme mteule Aleksander wa Masedonia. Baada Aleksander kuwa mfalme Aristoteli alirudi Athens 385/334 alipofundisha falsafa yake. Mnamo 323 bada ya kifo cha Aleksander Mkuu alipaswa kuondoka katika Athens kwa sababu wapinzani wa Masedonia waliongezeka nguvu akahamia Halki alipoaga dunia karibuni.
[hariri] Maandiko
Aristoteli alitunga kamusi ya falsafa na kitabu juu ya Pythagoras na kuna sehemu ya maandiko yale yaliyohifadhiwa. Lakini muhtasari zake alizotumia kwa masomo zilihifadhiwa zikakusanywa na wahariri wa baadaye na kutolewa kama maandiko yake.
Kati yao kuna maandiko juu ya mantiki, fizikia, falaki na metafizikia. Neno la "metafizikia" limetokana na maandiko ya Aristoteli kwa sababu dhana zake juu ya chanzo na tabia za vitu zilipangwa baada ya maelezo juu ya "fizikia" hivyo jina "meta-fizikia".
[hariri] Mafundisho
Aristoteli alukusanya elimu ya wakati wake akajaribu kuipanga katika utaratibu.
Mwenyewe alifundishwa na Plato lakini alitofautiana na mwalimu wake katika mafundisho juu ya tabia za vitu vyenyewe. Plato aliona ya kwamba ujuzi wote tunaonapata kupitia milango yetu ya utambuzi hukosa uhakika si kamili na ujuzi wa kweli unapatikana kwa njia ya roho inayoweza kuelewa kiini cha kitu wakati milango ya utambuzi inaona umbo la nje tu. Aristoteli alifikiri tofauti akaona utambuzi kupitia milango yetu ni muhimu zaidi na ujuizi hutegemea utazamaji wa mazingira.
Katika "metafizikia" yake kuna pia dhana zake juu ya "mwanzilishaji" au "mwenye mwendo wa kwanza". Aliona ya kwamba kila kitu kina mwendo kilichosababishwa na kitu kingina. Hivyo mantiki yake ilidai kuwepo kwa chanzo cha mwendo wote akakiita "mwendeshaji asiyeendeshwa" (kigir. proton kinoun akineton) au kwa lugha nyingine "chanzo asilia". Chanzo asili hiki kwake ni roho au dhana yenyewe (kigir. nous). Aristoteli aliweza kukiita pia "mungu".
Kati ya dhana zake za kudumu iko nadharia juu ya michezo tanzia inayotajwa mara nyingi kuhusu maigizo, filamu na hata michezo ya kompyuta ya leo. Kufuatana na Aristoteli mchezo tanzia huamsha hisi za watazamaji kama vile upendo, chuki, tumaini, huzuni au hofu. Ilhali mtazamaji anaingizwa katika hisi hizi roho yake husafishwa wakati wa kutazama mchezo.