Qurani
Kutoka Wikipedia
Lugha ya kidhehebu | Makala hiyo kuhusu "Qurani" inayohusu kichwa cha kidini inaonyesha lugha ya kidhehebu inayochanganya habari pamoja na mahubiri au mafundisho ya kidhehebu. Katika Kamusi Elezo tunahitaji lugha inayoeleza pia mafundisho na maoni kama habari bila kuyahubiri. Unaweza kusaidia kuiboresha kwa kubofya kitufe kilichoandikwa "hariri". Unaweza kuondoa sanduku hili baada ya kusahihisha makala. Ni vema kuacha mawazo yako kwa kifupi kwenye Ukurasa wa Majadiliano. Ikiwepo makala kuhusu Qurani inapatikana kwa lugha nyingine, unaweza kuitafsiri kwa Kiswahili. |
Qurani (pia Kurani au Korani) ni msahafu unaotumiwa na waumini wa Uislamu. Waislamu wanaamini kuwa yaliyomo ndani ya kitabu hicho ni ujumbe ambao mtume Muhammad alishushiwa na Mungu kupitia malaika Gabrieli. Wanavyoamini ujumbe huo ulimfikia Mtume Muhammad kwa ajili ya uongofu wa wanadamu kutoka kwa Allah (Mwenyezi Mungu). Kabla ya kuja ujumbe huu, Mwenyezi Mungu aliteremsha Wahyi kwa Mitume kadha wa kadha kama Nabii Musa (Taurati au Torati), Nabii Daudi (Zaburi), na Nabii Isa (au Yesu) (Injili).
Qurani kama maandishi yaliyotangulia kabla yake ya Taurati na Injili yaliteremshiwa Mitume wa Mwenyezi Mungu kupitia Malaika Jibrili ambaye ni mmojawapo wa Malaika wake wakubwa. Katika muda wa miaka 23 Qurani ilikuwa ikiteremshwa kidogo kidogo kama Wahyi kwa Muhammad kwa mujibu wa munasaba mbali mbali katika maisha ya Waislamu wa wakati wake, ili kuwatoa katika giza na kuwatia katika mwangaza, na kuwa ni uongofu wa watakaokuja baada yao.
Kuanzia wakati Muhammad alipokuwa na miaka 40 mpaka alipofikia umri wa miaka 63, Jibrili alikuwa akitumwa kwake kumteremshia hii Qurani yenye ujumbe kutoka kwa Mola wake uliokusanya maamrisho na makatazo na maelekezo na masimulizi mbalimbali za Umma zilizotangulia kwa ajili ya kuwaongoza Waislamu duniani, na kwa hiyo iliteremshwa katika muda wa miaka 23 mpaka Mtume Muhammad alipofariki dunia.
Kwa kuwa kila ufunuo au wahyi huteremshwa kwa Nabii fulani kwa lugha yake anayoitumia katika zama zake, kama vile Kiibrania kwa Mtume Musa na Kiaramu kwa Mtume Isa, vile vile Qurani iliteremshwa kwa lugha ya Muhammad ambayo ilikuwa ni Kiarabu. Pamoja na hayo, leo kuna tafsiri nyingi sana za Qurani kwa lugha mbalimbali ulimwenguni ili Waislamu wa makabila na jinsi tofautitofauti waweze kufahamu maana yake kwa lugha zao.
Qurani pamoja na Sunnah za Mtume Muhammad ndizo chanzo cha Sharia ya Kiislamu, na kutokana na maandishi haya, Waislamu wanajifunza kila aina ya Ibada (Sala, Saumu, Zaka na Hija), na kila aina ya Maingiliano (ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kadhalika). Tofauti kubwa baina ya maandishi haya ni kuwa Qurani ni maneno ya Mwenyezi Mungu kwa Waislamu au wanadamu kwa jumla, na Sunnah ni maneno na vitendo vya Mtume Muhammad katika uhai wake alipokuwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na yote mengine aliyoyaona na kuyasikia yakifanywa na Masahaba zake akawa hakuyapinga au kuyatoa makosa na yanachukuliwa kuwa ni mambo aliyoyakubali kuendelewa kufanywa.
Leo Qurani baada ya miaka zaidi ya elfu ni maneno na maandishi yale yale yaliyoachwa na Mtume Muhammad kwa Waislamu, nayo husomwa na kuzungumzwa na kusomeshwa na kuhubiriwa na kufasiriwa na kufanyiwa uchunguzi mbalimbali na Waislamu na wasiokuwa Waislamu, na kila kukicha mambo mengi katika maisha na sayansi yanagunduliwa yakiwa yanakubaliana na yale yaliyokuwemo ndani ya hii Qurani.
[hariri] Marejeo
- Online Quran Project (OQP)
- Multiple Translation of the Qur'an
- http://www.quranitukufu.com/
- http://www.islamicity.com/mosque/quran/
- http://www.islamicity.com/mosque/quran/#Translations
- http://www.grad.cgu.edu/~dadabhoa/webpage/quran.htm