Haile Selassie
Kutoka Wikipedia
Haile Selassie (23 Julai, 1892 – 27 Agosti, 1975) alikuwa Kaisari au Negus Negeste wa Ethiopia. Alizaliwa katika kijiji kiitwacho Ejersa. Aliitwa Ras Tafari Makonnen kabla ya kuwa mfalme. Jina lake la kifalme lina maana ya Utatu Mtakatifu. Pia anafahamika kwa jina la Simba wa Yuda, Mfalme wa wafalme (H.I.M). Baba yake alikuwa mkabaila Mwethiopia aliyeitwa Ras Makonnen akawa gavana wa Harar, familia yake ina watoto 11. Alikuwa mkristo muumini wa dhehebu la orthodoksi.
Yaliyomo |
[hariri] Gavana wa mikoa
Ras Tafari Makonnen alikuwa bado kijana alipopewa cheo cha gavana wa Sidamo mwaka 1907. 1911 akarithi nafasi ya gavana wa Harar. Wakati wa ugomvi kuhusu Negus Lij Iyasu (1913-1916) alisimama awali upande wa mfalme lakini alifaidika zaidi na uasi uliompindua Negus. Makabaila waliomwondoa Iyasu mwaka 1916 walimteua shangazi yake aliyekuwa binti wa Negus Negesti marehemu Menelik II Zauditu kuwa malkia wakaamua pia Ras Tafari awe mwangalizi wake.
[hariri] Mtawala na Negus Negeste
Kwa njia hii Ras Tafari akawa kiongozi muhimu zaidi nchini. 1928 Zauditu akampa cheo cha negus chini yake mwenyewe. Baada ya kifo cha Zauditu 1930 Ras Tafari akapokea taji la Kaisari pamoja na cheo cha Negus Negeste au mfalme wa wafalme wa Ethiopia akajiita Haile Selassie. Baada ya kupokea taji akafanya ziara ya Ulaya.
[hariri] Mwokozi wa Rastafari
Habari zake zikaenea kote duniani zikasababisha kutokea kwa dini mpya ya Rastafari kisiwani Jamaika waliopokea jina kutoka kwake. Watu weusi waliokuwa wajukuu wa watumwa wa asili ya Afrika walisikia mara ya kwanza ya kwamba Mwafrika aheshimiwa na wafalme wa Ulaya wakaona yeye ni mwokozi wa Mungu aliyerudi duniani kwa ajili ya watu weusi.
Haile Selassie alifukuzwa katika Ethiopia mwaka 1936 na mashambulio ya Italia dhidi ya Ethiopia akarudi 1941 kwa msaada wa Uingereza iliyoondoa Waiitalia nchini katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
[hariri] Sifa na kasoro za utawala wake
Utawala wa Haile Selassie wa baadaye ulimpa nafasi kubwa katika harakati ya uhuru wa Afrika na makao makuu ya Umoja wa Afrika yalijengwa Addis Ababa. Katika siasa yake ya ndani alishindwa kuendeleza nchi yake yake. Alikosa nguvu na nia ya kumaliza utawala wa kikabaila nchini uliosababisha umaskini mkali kati ya wakulima waliopaswa kuwaachia wakabaila sehemu ya mazao.
Kimataifa Haile Selassie aliheshimiwa sana lakini ndani ya nchi maendeleo yalikwama wanafunzi na wasomi wakikasirikia na wakulima maskini walikufa njaa mara kwa mara.
[hariri] Mapinduzi ya 1974 na kifo
Njaa kubwa ya 1972–73 katika majimbo ya Wollo na Tigray ikafuatwa na mapinduzi ya kijeshi ya 1974. Kamati ya kijeshi ya Derg ikamkamata Halie Selassie tar. 12 Septemba 1974.
Kifo cha Kaisari ikatangazwa tar. 28 Agosti 1975 na haieleweki kama aliuawa au kama alikufa kutokana na ugonjwa.
Baada ya kuondolewa kwa Derg mabaki ya maiti ya Kaisari yalipatikana mwaka 1992 chini ya sakafu ya choo cha jumba la kifalme alikokamatwa. Tar. 5 Novemba 2000 mabaki yale yalipewa mazishi ya kifalme katika kanisa kuu la Kiorthodoksi la Addis Ababa.