Chingis Khan
Kutoka Wikipedia
Chingis Khan (pia: Genghis Khan, * takriban 1162 – + 18 Agosti, 1227) alikuwa kiongozi wa Wamongolia aliyeunda Milki ya Wamongolia iliyoendelea kutawala eneo kubwa kuanzia China pamoja na Asia ya Kati hadi Urusi na Mashariki ya Kati.
Yaliyomo |
[hariri] Kuunganisha makabila ya Wamongolia
Alizaliwa kwa jina la Temujin kama mtoto wa chifu wa kabila la kimongolia. Wakati ule Wamongolia walikuwa wafugaji wahamiaji walioishi katika kaskazini ya nchi ya Mongolia ya leo. Walikuwa na makabila mengi yaliyoendelea kupigana kwa vita. Temujin alishiriki katika vita vingi akaendelea kuunganisha makabila mbalimbali. Tangu mwaka 1201 alikuwa na nguvu ya kutosha akashambulia mataifa ya jirani kama Watartari waliowahi kumwua babake na kuwashinda. Mwaka 1206 Temujin aliitisha mkutano wa viongozi wote wa Wamongolia waliomkubalia kama kiongozi mkuu na kumpa cheo cha "Chingis Khan" yaani mtawala mkubwa.
[hariri] Sheria za kimaandishi
Maazimio ya mkutano yalianzisha dola jipya ambamo Temujin alikuwa mtawala wa pekee mwenye madaraka ya kutunga sheria. Alitawala kwa msaada wa halmashauri iliyokuwa na mamake, kakaye na wana wake. Temujin alimwagiza mwana wake aliyejua mwandishi kuandika sheria zote za kale zilizohifadhiwa kwa kumbukumbu tu katika kitabu pamoja na amri na sheria mpya alizoendelea kutangaza. Nakala za kitabu hiki zilitumwa katika pande zote za milki yake. Sheria hizi zilimaliza utawala wa machifu waliowahi kuamua mambo kufuatana na hiari zao.
[hariri] Jeshi la kudumu
Temujin aliendelea kuanzisha jeshi kwa kutangaza sheria kila Mmongolia alipaswa kuwa mwanajeshi. Aliweza kuzawadisha askari wake kwa njia ya mali zilizotekwa vitani kama mateka. Yeye mwenyewe aliteua viongozi waliosimamia vikosi vya wanajeshi 1,000. Hapa hakuteua tena ndugu zake bali aliwachagua viongozi hao kulingana na uwezo na uaminifu.
Mwenyewe alikuwa na kikosi cha ulinzi wake wa wanajeshi wateule 10,000.
[hariri] Utawala
Kazi kubwa ya Temujin ilikuwa kujenga umoja na nidhamu. Wamogolia walizoea kuungana kwa vita lakini kuachana maungano na kufarakana kufuatana na hiari za machifu. Kwa kuunda jeshi la pamoja Temujin alikuwa na chombo cha kuunganisha makabila kwa njia ya kudumu kwa sababu machifu wa kale hawakuwa na nafasi tena katika muundo huo wakapungukiwa umuhimu.
Baada ya kutwaa milki za majirani alipata pia maafisa Wachina hasa waliokuwa na maarifa ya utawala aliweza kuanzisha utaratibu wa kodi na huduma.
Mwenyewe hakujua kuandika wala kusoma lakini alielewa umuhimu wa maandiko akaamuru kutungwa kwa mwandiko kwa ajili ya lugha ya Kimongolia.
Baada kuimarisha utawala wake kati ya China na Bahari ya Kaspi alijenga mji mkuu mpya ya Karakorum ilikuwa mji wa kwanza wa kudumu wa Mongolia. Kwa kazi kama utawala, biashara na ufundi alichukua watu kutoka sehemu mbalimbali ya milki yake; alitambua ya kwamba Wamongolia wenyewe walizoea ufugaji na vita tu kwa hiyo alitegemea wafanyabiashara Waislamu Waturuki na Waajemi, maafisa wa utawala na mafundi Wachina na wataalamu Wakristo.
[hariri] Upanuzi
Baada ya kuunganisha makabila ya wafugaji Temujin aliongoza jeshi lake dhidi ya milki ya China katika kusini. Kuanzia mwaka 1211 alivuka ukuta mkubwa wa China kwa jeshi la askari 100,000. 1215 alitwaa Beijing na kuanzia 1219 hata milki ya Korea ilianza kumlipia hongo.
Mwaka 1218 kulitokea matatizo na majirani wa Khorezmu upande wa magharibi; msafara wa Kimongolia uliwahi kushambuliwa na mabalozi waliotumwa huku kupeleleza hali waliuawa. Kwa hiyo Temujin aliitia mkutano wa viongozi wa milki yake wakaamua kushambulia Khorezmu. Mkutano uleule ulimkubali pia mwana wa tatu Ugedai kama mrithi wa Temujin atakayemfuata kama Khan mkuu.
1219/1220 Wamongolia walimshinda mfalme wa Khorezmu wakaangamiza miji ya ufalme huu na kuua watu wengi. Vikosi wa jeshi hili viliendelea upande wa magharibi na kuangamiza nchi za Warusi na sehemu za Kaukazi.
[hariri] Kifo na urithi
Mwaka 1227 Chingis Khan alikufa akiwa mzee; wengine husema ya kwamba sababu ya kifo ilikuwa anguko kutoka farasi; wengine husema ya kwamba binti wa mfalme aliyeuawa na Temujin alilipiza kisasi kwa kumdunga kwa kisu. Kaburi lake lilifichwa na walinzi wake kufuatana na desturi ya Wamongolia haijulikana hadi leo. Inasemekana ya kwamba wapandaji farasi 1,000 walikanyaga sehemu ya kaburi kwa miguu ya farasi zao halafu waliuawa wenyewe baada ya kuleta taarifa ya kwamba walitimiza kazi ya kumzika Chingis Khan.
Wafuasi wake waliendela kupanusha milki. China yote pamoja na Urusi zilikua majimbo ya milki na milki ya Wamongolia ilkuwa milki kubwa katika historia ya dunia.
Kwa watu wengi Chingis Khan ni sawa na ushindi katili na ya kinyama. Lakhi za watu waliuawa na wanajeshi wake. Aliposhinda taifa la Watartari aliamuru watu wote wenye urefu juu ya futi nne wauawe yaani watu wazima wote. Wamongolia siku hizi wanamwona kama Baba yao wa Taifa. Alitumia miaka mingi kuunganisha na kueneza makabila ya watu wahamiaji wa Mongolia.
Baadhi ya wanahistoria wanasema kwamba alikuwa na kichwa kizuri cha kijeshi kuliko karibu watu wote wengine katika historia ya dunia.
[hariri] Viungo vya nje