Milki ya Osmani
Kutoka Wikipedia
Milki ya Osmani ilikuwa dola kubwa lililotawala upande wa mashariki wa Mediteranea pamoja na nchi nyingi za Mashariki ya Kati kwa karne nyingi kati ya karne ya 14 hadi 1922.
Milki ilianzishwa na Waturuki Waosmani ikachukua nafasi ya ukhalifa wa Waabbasi na Milki ya Bizanti.
Mji wake mkuu ulikuwa Konstantinopoli (leo: Istanbul) na mtawala wake mkuu alikuwa Sultani wa Waosmani. Imani rasmi ya milki ilikuwa Uislamu hata kama katika maeneo mengi idadi kubwa ya wakazi walikuwa Wakristo.
Tabaka ya viongozi wa kisiasa na kijeshi walikuwa Waosmani walikouwa Waturuki pamoja na mchanganyiko wa Waislamu kutoka sehemu zote za milki yao hasa Balkani. Kwenye uwanja wa uchumi na utawala Waosmani walitumia sana Wakristo Wagiriki na Waarmenia.
Yaliyomo |
[hariri] Chanzo
Milki ilianza kama eneo ndogo la kabila ya Kiturki katika Anatolia chini ya chifu Osmani I likaendelea kupanua hasa kwa kutwaa sehemu za milki ya Bizanti upande wa Asia na Ulaya ya Kusini-Mashariki.
[hariri] Kutwaa kwa Bizanti
1453 Waosmani walitwaa mji wa Konstantinopoli na kumaliza Milki ya Bizanti wakifanya mji kuwa mji mkuu wao.
Katika karne ya 16 Waosmani waliendelea kupanua kenye Balkani upande wa Ulaya, Kaukazi, Mesopotamia upande wa Asia na katika Afrika ya Kaskazini.
[hariri] Ukhalifa
Baada ya kushinda Wamamaluki katika Misri sultani (Selim I) alikuwa pia mkuu wa Makka na Madina akaendelea kujipatia cheo cha khalifa.
Kilele cha enzi yake ilikuwa katika karne za 16 hadi 17. Mwaka 1683 Waosmani walijaribu mara ya pili kuvamia Austria na kuteka Vienna lakini walishindwa. Kuanzia tukio lile athira yao katika Ulaya ilianza kupungua.
[hariri] Mzee mgonjwa wa Ulaya
Katika karne ya 18 nchi za Ulaya zilipita Milki ya Osmani kiteknolojia, kiuchumi na polepole pia kijeshi.
Wakati wa karne ya 19 Milki ya Osmani ikaitwa "Mzee mgonjwa wa Ulaya" (pia: "Mgonjwa wa Bosporus") na ilikuwa hasa mashindano kati ya Urusi, Ufaransa, Uingereza na Austria-Hungaria yaliyozuia kudhindwa kwake kwa sababu kila nchi kubwa ya Ulaya ilihofia ya kwamba nchi nyingine ingejipatia sehemu kubwa za Milki ya Osmani hivyo walizuiliana. Lakini nguvu yake iliendelea kufifia.
Kwenye mwisho wa karne ya 19 Masultani walijaribu kutekeleza matengenezo mablimbali ya muundo wa kisiasa na kiuchumi lakini mabadiliko yalitokea polepole.
[hariri] Mwisho wa Waosmani
Mwisho wa milki ilikuja katika vita mwanzoni wa karne ya 20. Vita za Balkani ziliondoa karibu nchi zote upande wa Ulaya kutoka utawala wa Waosmani. Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ilimaliza milki hii. Serikali iliamua kujiunga na Ujerumani na Austria-Hungaria dhidi ya Urusi, Uingereza na Ufaransa.
1918 jeshi na dola zikaporomoka kabisa. Milki ikagawiwa na washindi wa vita. Sehemu za Kiarabu zikawa nchi lindwa za Uingereza na Ufaransa. Katika maeneo yaliyobaki nchi mpya ya Uturuki ikaanzishwa.