Bahari ya Baltiki
Kutoka Wikipedia
Bahari ya Baltiki ni bahari ya kando ya Atlantiki katika Ulaya ya Kaskazini. Imezungukwa na nchi kavu pande zote isipokuwa kuna mlango mwembamba wa kuiunganisha na Bahari ya Kaskazini kati ya Denmark na Uswidi.
Yaliyomo |
[hariri] Mipaka yake
Bahari ya Baltiki imepakana na nchi za Uswidi, Ufini, Urusi, Estonia, Latvia, Lituanya, Poland, Ujerumani na Denmark. Sehemu ya kaskazini kabisa iko mpakani wa Uswidi na Ufini katika Ghuba ya Bottnia, sehemu ya mashariki kabisa katika Ghuba ya Ufini kwenye mji wa Sankt Petersburg. Sehemu ya kusini iko kwenye mpaka wa Poland na Ujerumani na sehemu ya magharibi kwa mji wa Flensburg karibu na mpaka wa Ujerumani na Denmark. Njia ya kuunganisha Baltiki na Bahari ya Kaskazini ni mlango wa bahari ya Kattegat na Skagerak. Mwanzoni wa Kattegat njia inapita kwenye visiwa vya Denmark na kuigawa katika njia tatu ndogo zinazoitwa Oresund, Belt Kubwa (Kidenmark: Storebælt) na Belt Ndogo (Kidenmark: Lillebælt).
[hariri] Zama za Barafu
Kijiografia Baltiki ni mabaki ya Zama za Barafu iliyopita. Takriban miaka 12,000 iliyopita Ulaya yote ya Kaskazini ilifunikwa na ganda la barafu lenye unene wa mamia ya mita. Wakati wa kupungua kwa ubaridi barafu ilianza kuyeyuka na kusababisha kutokea kwa ziwa kubwa sana ambalo ni mwanzo wa Baltiki. Ziwa hili lilipata njia ya kujifungua kwa bahari na kiasi cha maji ya chumvi yaliingia ndani. Hivyo maji ya Baltiki ni mchanganyiko wa maji ya chumvi na maji matamu. Kiasi cha chumvi ndani ya maji yake ni kidogo kulingana na maji ya bahari ya kawaida.
[hariri] Bahari yenye chumvi kidogo
Kiasi cha chumvi ni kikubwa zaidi kwenye kina kuliko kwenye maji ya juu. Wakati maji yenye chumvi kidogo inatoka kwenye Kattegat kuelekea Bahari ya Kaskazini kuna pia mwendo wa maji ya chumvi chini yake ya kuingia katika Baltiki. Maji ya chumvi ni nzito zaidi kuliko maji matamu hivyo inakaa kwenye vilindi vya bahari na kuwa na mwendo wa kuingia ilhali wakati huohuo maji ambayo ni matamu zaidi yanapita juu yake kutoka Baltiki.
[hariri] Mito ya Baltiki
Mito mikubwa inaingia katika Baltiki na kusababisha mwendo wa maji ya kutoka katika Kattegat na kuingia Atlantiki. Kati ya mito hii ni: Oder, Vistula, Neman, Daugava na Neva.
[hariri] Visiwa na funguvisiwa
- Funguvisiwa ya Åland (Ufini, eneo la kujitawala ndani ya Ufini)
- Funguvisiwa ya Turku (Ufini)
- Hailuoto (Ufini)
- Valassaaret (Ufini)
- Gotland (Uswidi)
- Öland (Uswidi)
- Funguvisiwa ya Stockholm (Uswidi)
- Hiiumaa (Estonia)
- Saaremaa (Estonia)
- Muhu (Estonia)
- Kotlin (Urusi)
- Wolin (Poland)
- Usedom au Uznam (imegawiwa kati ya Ujerumani na Poland)
- Rügen (Ujerumani)
- Bornholm (Denmark)
[hariri] Miji
Miji mikubwa kando la Baltiki:
- Stockholm (Uswidi) 774,411 (pamoja na mitaa ya nje 1,729,274)
- Malmö (Uswidi) 259,579
- Helsinki (Ufini) 559,716 (pamoja na mitaa ya nje 1,200,000)
- Turku (Ufini) 175,000
- Sankt Petersburg (Urusi) 4,700,000
- Kaliningrad (Urusi) 400,000
- Riga (Latvia) 760,000
- Tallinn (Estonia) 401,774
- Klaipėda (Lituanya) 194,400
- Gdańsk (Poland) 462,700 (pamoja na mitaa ya nje 1,041,000)
- Szczecin (Poland) 413,600
- Gdynia (Poland) 255,600
- Kiel (Ujerumani) 250,000
- Lübeck (Ujerumani) 216,100
- Rostock (Ujerumani) 212,700
- Copenhagen (Denmark) 502,204 (pamoja na mitaa ya nje 1,823,109)