Waraka kwa Waebrania
Kutoka Wikipedia
Miaka ya 60 B.K. Mkristo mwenye asili ya Kiyahudi na elimu ya Kiyunani, aliwaandikia Wakristo wa Kiyahudi wenzake si barua hasa bali hotuba kamili iliyoambatanishwa na kipande cha barua.
Hali iliyosababisha uandishi ni baadhi yao kuvutiwa tena na dini yao asili na ibada zake hekaluni: kishawishi kilikuwa kikubwa hasa kwa sababu Kanisa lilikuwa bado mwanzoni, bila ya mahali maalumu pa kusali wala ibada za fahari.
Mwandishi aliwaonya kuwa wakimuasi Yesu hawamrudii Mungu aliye hai, aliyejifunua hasa katika Mwanae, bali wanamsulubisha tena kwa makusudi mazima na kustahili tu moto wa milele.
Sehemu kubwa ya maandishi hayo inalinganisha Yesu Kristo na ukuhani wake katika hekalu la mbinguni upande mmoja, na ukuhani wa Agano la Kale huko Yerusalemu upande mwingine.
Hivyo mwandishi alielekeza safari ya kiroho katika imani inayofanana na ile ya watakatifu wa Agano la Kale.
Kwa kuwa lengo halikuwa la kinadharia, bali kuhimiza uaminifu, kila baada ya kuchambua ukweli fulani aliongeza mawaidha ya kufaa.
Ubora wake ni kulinganisha mambo ya kale na utimilifu wake katika Agano Jipya, pia kuthibitisha ukuu wa Kristo kama kuhani wa milele (Eb 1:1-2:4; 4:11-5:10; 7:1-8:13; 10:19-11:40; 13:22-25).