Johannes Gutenberg
Kutoka Wikipedia
Johannes Gensfleisch zur Laden zum Gutenberg anayejulikana kifupi kama Johannes Gutenberg) (mnamo 1400s - 3 Februari 1468) alikuwa fundi dhahabu na mvumbuzi kutoka Ujerumani aliyebuni teknolojia ya kuchapa vitabu kwa herufi za kusogezeka. Alitengeneza mashine ya kwanza ya kuchapa vitabu, alibuni aloi ya kufaa herufi kwa mashine yake pamoja na wino. Alitengeneza pia kifaa kilichomwezesha kusubu herufi za metali haraka.
Yaliyomo |
[hariri] Vitabu kabla ya Gutenberg
Kabla ya Gutenberg vitabu vingi viliandikwa kwa mkono. Kunakili kitabu kimoja kama Biblia kwa mkono kulichukua angalau mwaka mmoja.
Teknolojia ya kuchapisha vitabu ilipatikana tayari lakini haikuridhika. Kwa kawaida ukurasa wote ulichorwa halafu kukatwa katika ubao. Ubao ulipakwa wino na karatasi zilisukumwa kwa ubao huu. Udhaifu ilikuwa kwanza kazi kubwa ya kutengeneza bao halafo bao hizi hazikudumu sana.
[hariri] Biblia ya Gutenberg
Kazi ya kwanza ya Gutenberg ilikuwa Biblia. Imesifiwa kama kazi bora ya kifundi na kisanii.
[hariri] Teknolojia mpya
Mbinu ya Gutenberg ilikuwa kutumia metali badala ya ubao na kuunganisha mwandiko wa ukurasa kwa herufi zilizoandaliwa moja-moja halafu kuunganishwa kwa mstari na ukurasa. Alitangulia kutengeneza herufi kwa kumwaga aloi ya plumbi (metali ya risasi), stani na antimoni katika kalibu ilipopoa. Kwa njia aliweza kusubu herufi nyingi zilizokuwa sawa kabisa tofauti na herufi zilizokatwa kwa mkono katika ubao. Baada kupanga herufi na kuzibana aliweza kuchapisha ukurasa mara nyingi jinsi ilivyohitajika. Aliweza pia kufungua mbano wa ukurasa na kutumia herufi kwa kazi nyingine au kutunza ukurasa kwa marudio yaliyotarajiwa.
Pamoja na hayo alibuni mgandamizo iliyokuwa mashine bora ya kuchapa vitabu.
[hariri] Matokeo ya kazi ya Gutenberg
Mavumbuzi hivi vyote vilianzisha mapinduzi ya teknolojia na utamaduni. Vitabu vilianza kupatikana haraka kuliko awali. Bei ya vitabu ilishuka. Baada ya kuongezeka kwa vitabu watu wengi zaidi walianza kusoma. Shule zilienea kushinda zamani.
Teknolojia ya Gutenberg iliwezesha harakati ya matenegenzo ya kiprotestanti iliyoanza na Martin Luther mwaka 1517. Maandiko ya Luther yalisambaa haraka kote Ulaya. Maandiko ya wafuasi na wapinzani wake yalifuata. Watu wengi walishiriki na kufuatilia habari hizi.
Gutenberg amehesabiwa kati ya watu 100 wa istoria ya dunia waliokuwa na athira kubwa. Gazeti la Newsweek alimteua kama "Mtu wa milenia 1000-2000".