Timur
Kutoka Wikipedia
Timur (*8 Aprili 1336 - † 19 Februari 1405) alikuwa kiongozi mwislamu wa Waturuki na Wamongolia wa Asia ya Kati wakati wa karne ya 14 aliyeanzisha milki ya Watimuri.
Jina lake kamili ilikuwa Timur bin Taraghay Barlas kutokana na neno la Kichagatai تیمور "chuma". Alijulikana pia kama Timur-e Lang yaani "Timur mlemavu" au Tamerlan. Aliitwa pia "Timur Mkuu".
Alizaliwa mjini Kesh (leo: Sachrisabz) karibu na Samarkand katika Uzbekistan. Aliaga dunia mjini Otrar katika Kazakhstan ya leo.
Akianza kama chifu wa kabila ndogo alipanda ngazi katika utumishi wa watawala wa Chagatai na kuchukua nafasi yao. Baada ya kuoa binti wa ukoo wa Jingis Khan alilenga kurudia milki ya Jingis Khan kwa umbo la Kiislamu. Timur mwenyewe alikuwa Mwislamu mkali aliyelazimisha Wamongolia wote wa eneo lake kukubali Uislamu. Alipenda pia mila na desturi za Wamongolia wa kale kabla ya kugeukia Uislamu.
Kwa njia ya vita vingi alipanusha milki yake. Alihofiwa kama kiongozi mkali bila huruma kwa maadui na wapinzani. Vita zake zakumbukwa kwa sababu ya idadi kubwa ya watu waliochinjwa na wanajeshi wake.
Kuna mifano mingi ya unyama wake. Baada ya jeshi lake kutwaa mji wa Isfahan (Uajemi) minara 28 ya vichwa vilihesabiwa, jumla la watu 70,000 walichinjwa. Baada ya kutwaa Baghdad 1401 aliamuru maandamano ya wanajeshi mbele yake akadai kila askari ashike vichwa viwili vilivyokatwa.
Alichukia hasa Wakristo katika milki yake kwa sababu sehemu ya Wamongolia na Waturuki walifuata Ukristo wa Kinestorio. Ukristo wa Asia ya Kati ulipungukiwa mno na kupotea kabisa katika nchi kadhaa chini ya Timur. Lakini alichukia pia Wahindu akichinja wafungwa 100,000 wakati wa kushambulia Delhi mwaka 1398.
Baada ya kifo chake miliki iliporomoka haraka kwa sababu ilijengwa kwa hofu bila utaratibu wa kiutawala.