Oreste Baratieri
Kutoka Wikipedia
Oreste Baratieri (13 Novemba, 1841 – 7 Agosti, 1901) alikuwa jenerali katika jeshi la Italia na gavana wa koloni ya Eritrea aliyeongoza Waitalia katika mapigano ya Adowa waliposhindwa vibaya na Ethiopia.
Baratieri alikuwa mwenyeji wa jimbo la Tirol upande wa kaskazini wa Italia. Alishiriki katika mapigano ya vita ya maungano ya Italia chini ya Guiseppe Garibaldi miaka ya 1860 na 1861.
1891 alipewa cheo cha jenerali na kuwa mkuu wa jeshi la Italia katika Eritrea. 1892 alikuwa pia gavana. Baratieri aliongoza wanajeshi wake katika ushindi wa mapigano mbalimbali dhidi ya vikosi vya watemi na makabila ya Ethiopia.
1895 alipokea amri za serikali yake ya kushambulia Ethiopia baada ya Negus Menelik II alikana mkataba wa Wuchale. Baratieri alitembelea Italia na kuwahutubia wananchi akiwaahidi atamleta Menelik kama mfungwa.
Oktoba 1895 Baratieri alivuka mto Mareb na kuingia Ethiopia. Baada ya mapigano ya kwanza alijifunza kuhusu jeshi kubwa la Menelik akaamua kusubiri hadi akiba za chakula cha Waethiopia ziishe. Lakini serikali ya waziri mkuu Crispi alitaka kutangaza ushindi ikamwamuru Baratieri ashambulie mara moja.
Shindikizo hili lilisababisha mapigano ya Adowa ambako wanajeshi 17,000 Waitalia na Waeritrea walipigwa vibaya na jeshi la Menelik lenye wanajeshi kati 80,000 hadi 100,000. Waitalia walipoteza wanajeshi 10,000 waliokufa au kutekwa wafungwa na adui pamoja na mizinga yote na bunduki 11,000. Wengine waliweza kukimbia na kujiokoa kwenda Eritrea.
Baratieri aliweza kujiokoa lakini alisimamishwa mbele ya mahakama ya kijeshi iliyoona ya kwamba alifanya makosa lakini hana hatia. Mwaka 1897 alijiondoa madarakani na kuchukua pensheni yake. Aliishi katika Tirol ya Kiaustria alipoaga dunia tarehe 7 Agosti 1901 mjini Sterzing-Vipiteno.