Barua ya kwanza kwa Wakorintho
Kutoka Wikipedia
Kutoka Korintho (Ugiriki) habari za kusikitisha zilimfikia Mtume Paulo akiwa Efeso (pengine mwaka 57): katika Kanisa kulikuwa na shaka kuhusu [[[imani]], mafarakano, upinzani wa Wakristo wa Kiyahudi dhidi yake, na makwazo.
Basi mwaka mzima akawa na mahangaiko kwa Wakorintho akawaandikia walau barua nne au tano, ingawa sisi tunazo mbili tu; pengine sehemu za baadhi yake zimeshonwa ndani ya 2Kor.
Mpangilio wa barua ya kwanza una salamu na shukrani, halafu hukumu juu ya matatizo ya Wakristo hasa kufarakana (1Kor 1:10-16; 2:1-4:16), kuzini na kushtakiana mahakamani (1Kor 5-6).
Baada ya hapo akaanza kujibu maswali yao mbalimbali: kuhusu ndoa na useja (1Kor 7), nyama zilizotolewa sadaka kwa miungu (1Kor 8:1-11:1), mwenendo katika ibada na karama (1Kor 11:20-33; 12:4-13:13; 14:18-40), na hatimaye ufufuko wa wafu (1Kor 15:1-28,33-49).
Mwishoni kuna maagizo, taarifa na salamu mbalimbali (1Kor 16:1-4).
Kati ya mambo mengi muhimu, barua hiyo inatunza simulizi la kwanza la karamu ya mwisho ya Bwana Yesu (11:23-25) na kanuni ya imani ya kwanza inayoorodhesha pia matokeo ya Yesu Kristo Mfufuka (15:3-8).