Abrahamu
Kutoka Wikipedia
Abrahamu (pia: Ibrahimu na awali Abram) huheshimiwa katika Uyahudi, Ukristo na Uislamu kama kielelezo cha mtu wa imani, rafiki wa Mungu. Aliishi miaka 1800 hivi K.K. huko Mashariki ya Kati. [Image:Offerismail.jpg|thumb|Picha ya Abrahamu katika Kurani]]
[hariri] Abrahamu katika Biblia
Habari zake zinapatikana kwanza katika Biblia, hasa kitabu cha Mwanzo sura 11-25, halafu zinafikiriwa katika vitabu vilivyofuata, hata Agano Jipya.
Humo anatambulishwa kama mfugaji kutoka Mesopotamia (Iraq), aliyesikia sauti ya Mungu ikimwamuru aondoke katika nchi yake na kusafiri kwenda nchi atakayoonyeshwa: katika nchi hiyo ya ahadi atabarikiwa na kupewa watoto pamoja na mali. Abrahamu akafuata maagizo yote pamoja na mke wake Sarai (baadaye Sara) na kwa hivyo anasifiwa kuwa kielelezo cha mtu anayeitikia neno la Mungu na kuiamini hata hajaona kitu bado. Ndiye mwanzo wa taifa teule la Mungu na baba wa waamini wote.
Abram, ingawa alizaliwa Mesopotamia baada ya watu wa huko kustaarabika na kubuni uandishi, aliishi kwa kuhamahama pamoja na mifugo yake: akipitia Sirya alifikia nchi ya Kanaani aliyoahidiwa na Mwenyezi Mungu akashukia Misri kwa muda (Mwa 12).
Lakini safari yake muhimu zaidi ni ile ya imani, kwa kuwa aliongozwa na Mungu siku kwa siku, katika mazuri na magumu, akisadiki ahadi zake za ajabu (Eb 11:8-19). Mchungaji huyo alikubali Mungu amchunge maisha yake yote, akamfuata bila ya wasiwasi, akituachia mfano bora wa kumshika mkono Mungu daima bila ya hofu.
Hasa Mungu alimuahidia uzao mkubwa kama nyota za mbinguni, naye akaamini ingawa alikuwa hajapata hata mtoto mmoja: ndiyo imani iliyompendeza sana Mungu (Mwa 15:1-6).
Lakini Abrahamu anazeeka pamoja na Sarai bila ya kuzaa watoto. Baada ya kusubiri muda mrefu mno Sarai akamwambia azaliane na Hagar aliye mtumishi wa kike. Mwana huyu wa Hagar akaitwa Ismaeli (Mwa 16:1-15). Lakini baadaye kukawa na fitina kati ya Sarai na Hagar hivyo huyo akafukuzwa pamoja na mtoto. Biblia inamtaja Ismaeli kama babu ya Waarabu wote.
Mwa 18 inamchora Abrahamu kama mtu mkarimu sana kwa wageni, rafiki wa Mungu anayestahili kuambiwa yote, mwenye huruma, busara na unyenyekevu katika sala. Wageni wake watatu ambao ni kama mtu mmoja tu kwa Wakristo wanadokeza Utatu Mtakatifu. Mungu alimdai Abrahamu asadiki kwamba anaweza yote kama atakavyomdai Bikira Maria (Lk 1:17), naye alidumu kumuomba awahurumie waovu kwa ajili ya waadilifu (Yak 5:16).
Mwa 19 inatuchorea uovu wa watu ambao huko Sodoma ulizidi hata kumdai Mungu alipe kisasi. Lakini kati yao mwadilifu akaokolewa, isipokuwa mke wake akaja kuadhibiwa kwa sababu aliangalia nyuma kinyume cha agizo la Bwana (Lk 17:28-33).
Hatimaye Sara pia akashika mimba na kumzaa mtoto Isaka. Mwa 21:1-21 inatusimulia jinsi Mungu alivyotimiza ahadi yake kwa kumjalia Sara amzalie Abrahamu mtoto huyo katika uzee na utasa. Isaka ni mtoto wa imani, si wa mwili, naye ni huru, tofauti na Ismaeli mtoto wa mtumwa ambaye hastahili kurithi pamoja na mdogo wake. Isaka, baba wa Israeli alipata baraka kuu, naye ni mfano wetu watu wa Agano Jipya. Ismaeli alibarikiwa pia kwa ajili ya baba yake, naye ni mfano wa Agano la Kale ambapo watu wanategemea mambo ya kimwili (kutahiriwa, kunawa, kubagua vyakula n.k.) na hivyo ni watumwa (Gal 4:21-5:1).
Mwa 22:1-19 inatuletea habari ya kusisimua kuhusu sadaka ambayo Mungu alimdai Abrahamu, yaani kumchinja Isaka. Ni kimoja kati ya vilele vya imani ya binadamu, imani inayoonyeshwa kwa matendo ya utiifu (Yak 2:21-22). Abrahamu hakusita kumrudishia Mungu kile alichopewa, akaondoka alfajiri akasafiri mpaka mahali alipoambiwa (Wayahudi wanaamini mlima huo ndipo walipojenga hekalu la Yerusalemu). Kwa niaba ya waamini wote Abrahamu alikuwa tayari kumchinjia Mungu mwanae pekee ampendaye. Lakini kadiri ya Injili atakayemtoa kweli Mwana pekee ni Mungu Baba (Yoh 3:16). Yesu ndiye mwanakondoo aliyeuliziwa na Isaka na ambaye Mungu akajipatia juu ya mlima Kalivari alioupanda huku amejitwika sio kuni bali mti wa msalaba. Abrahamu aliamini uwezo wa Mungu juu ya mauti na hasa uaminifu wake kwa ahadi alizompa: kwa hiyo akarudishiwa mwana hai kama mfano wa ufufuko, na katika yeye, yaani katika mzawa wake, watu wote wakabarikiwa. Maisha ya imani yanadai daima sadaka, hasa ya mambo yanayopendwa zaidi (Rom 12:1-2): ndiyo njia ya kujaliwa baraka zinazopita ubinadamu wetu.
Mwa 24 inasimulia kirefu jinsi Abrahamu kabla hajafa alivyomfanyia mpango wa ndoa Isaka kufuatana na mila zao, ila alikataza kabisa asirudi kwao, bali kwa vyovyote abaki katika nchi ile aliyoahidiwa na Mungu. Hivyo imani izidi kuongoza uzao wake kama ilivyomuongoza mwenyewe. Isaka akawa mrithi wa Abrahamu. Watoto 12 wa mwanae Yakobo ni chanzo cha makabila 12 wa Israeli. Hivyo Abrahamu huangaliwa pia kama babu wa Wayahudi wote.
[hariri] Ibrahimu katika Qurani
Hata katika Uislamu Abrahamu-Ibrahimu ni kielelezo muhimu cha imani. Kwenye Qurani hutajwa mara kwa mara katika sura 25 na mistari 245. Kwa jumla habari zake zimekuwa tofauti na taarifa za Biblia lakini heshima inalingana.
Habari zinazosumuliwa katika Biblia juu ya Isaka, baba wa Waisraeli, pengine hurudia kwenye Qurani na kutafsiriwa na wengi kuwa zilimhusu Ismaeli, kaka yake na baba wa Waarabu. Anaaminiwa kuwa alijenga Kaaba kama msikiti.