Orientalium Ecclesiarum
Kutoka Wikipedia
Mtaguso wa pili wa Vatikano ulizingatia hali duni ya Makanisa Katoliki ya Mashariki ukaamua kuirekebisha.
Kwanza ulitamka kuwa yanastahili kuheshimiwa sana pamoja na mambo yote (liturujia, teolojia, sheria za Kanisa, miundo n.k.) kama sehemu ya hazina ya Kimungu iliyokabidhiwa kwa Kanisa.
Liturujia zitunzwe kiaminifu na kurekebishwa kama zimeachana na mapokeo ya Mashariki, hasa sakramenti zirudi kufuata taratibu asili.
Mashirika ya Kilatini yajitahidi kuanzisha jumuia za Mashariki. Madhehebu yoyote ya Kikatoliki yana haki na wajibu sawa hata kuhusu uenezaji Injili duniani kote.
Wachungaji wa hayo yote wazoee kushirikiana, na wanaojiandaa kupata upadri waelimishwe juu ya uhusiano kati ya madhehebu hayo.
Waamini wa Mashariki wapatiwe mapadri na maaskofu wao popote wanapohitaji.
Waortodoksi wakijiunga na Kanisa Katoliki waendelee kufuata madhehebu yao, na wenye daraja kati yao waendelee kuitumia.
Kutokana na umuhimu wa patriarki kwao, hadhi na haki zake zirudishwe kama kabla ya utengano na Waortodoksi, na Makanisa yasiyo naye yafikiriwe.
Hatimaye hati hiyo inahimiza Wakatoliki wa Mashariki kushughulikia ekumeni hasa upande wa Waortodoksi, ikiruhusu kutoleana nao sakramenti kadhaa na mengineyo.