Morogoro (mji)
Kutoka Wikipedia
Mji wa Morogoro ni mji nchini Tanzania uliopo takriban kilomita 200 upande wa magharibi wa Dar es Salaam ambao ni makao makuu ya Mkoa wa Morogoro. Kulingana na sensa ya mwaka 2002, idadi ya wakazi wake ilihesabiwa kuwa 228,863 [1].
Mji uko kando ya milima ya Uluguru. Ni kitovu cha viwanda vya mazao na mahali pa Chuo Kikuu cha Sokoine.
Morogoro ni njiapanda ya barabara muhimu za Dar es Salaam - Mbeya na Dar es Salaam - Dodoma zinazokutana hapa. Pana pia kituo cha reli ya kati kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, Mwanza na Kigoma. Reli ya TAZARA hupita nje ya mji mbali kidogo.