Kilimia
Kutoka Wikipedia
Kilimia (pia: thuria kutokana na Kar. "ثریا") ni fungunyota katika kundi la nyota la Taurus (fahali). Jina la kisayansi ni "M45" (katika orodha ya Messier).
[hariri] Tabia za kifalaki
Kwa macho nyota sita hadi saba zaonekana vizuri sana na hadi 14 kwa jumla. Lakini kwa darubini kilimia ni fungunyota yenye nyota 1,200. Umbali wake na jua letu ni miaka ya nuru 410. Umri wake hukadiriwa kuwa miaka milioni 125.
[hariri] Ishara ya mvua
Fungunyota hii inaonekana vizuri kabisa kwa macho. Inaanza kuonekana angani masaa ya mwanzo wa usiku katika miezi kuanzia Oktoba. Hivyo kuonekana kwake imechukuliwa na wazee katika Afrika Mashariki kama kalenda ya kuandaa mashamba na kilimo kwa sababu mvua umekaribia. Hii ni sababu ya kupewa jina la "kilimia" kutokana na "kulima, kilimo".
Methali ifuatayo yadokeza uhusiano huu kati ya kuonekana kwa kilimia na mvua: "Kilimia kikizama kwa jua huzuka kwa mvua, kikizama kwa mvua huzuka kwa jua."
Waswahili walitumia pia jina la kiarabu la "thuria" (ثریا).
Nafasi ya nyota kama ishara za kalenda zinapungua kwa sababu nyakati za kuonekana au kuzama hubadilika polepole baada ya karne kadhaa kutokana na mwendo wa mfumo wa jua letu angani.
[hariri] Kilimia katika mapokeo ya tamaduni mbalimbali
Kwa lugha nyingi kilimia huitwa kwa jina kama "nyota saba" kwa sababu ni takriban nyota 6 hadi saba zinazoonekana vizuri kwa macho. Mtu mwenye macho mazuri sana ataona hata 9 hadi 14.
Kilimia ni pamoja na Orioni kati ya makundi ya nyota yanayotajwa mara kadhaa katika Biblia (Ayubu 9:9 na 38:31; Amosi 5:8).
Kuonekana kwao kulikuwa alama ya kalenda katika tamaduni nyingi kama kati ya Wakelti, Wagermanik, Wazteki na wengine.
Wagiriki wa Kale walikiita "Pleiadi" na kusimulia hadithi ya mabinti saba wazuri waliopelekwa angani na mungu Zeus ili kuwalinda dhidi ya tamaa za mvindaji Orion. Miaka 2500 iliyopita ilionekana Ugiriki jioni wakati wa Mei hivyo ilikuwa ishara ya kuanza mavuno. Kuzama wakati ule mwezi wa Novemba kulikuwa ishara ya kulima mashamba kabla ya baridi.
Makala hiyo kuhusu "Kilimia" bado ni mbegu. Unaweza kusaidia kuikuza kwa kubofya kitufe kilichoandikwa "hariri". Ikiwepo makala kuhusu Kilimia kwa lugha nyingine, unaweza kuitafsiri kwa Kiswahili. |