Spika
Kutoka Wikipedia
Spika (kutoka Kiingereza "speaker" msemaji) ni cheo cha mwenyekiti wa bunge katika nchi zinazofuata urithi wa kisiasa wa Uingereza. Nchi nyingi zilizokuwa koloni za Uingereza kama vile Marekani, Uhindi, Tanzania, Kenya, Nigeria, Australia au New Zealand huwa na cheo hiki hasa zikitumia lugha ya Kiingereza kama lugha rasmi. Neno la Kiingereza limepokelewa pia katika lugha ya Kiswahili.
Katika nchi zisizo na urithi wa Kiingereza vyeo kama mwenyekiti au rais wa bunge hutumiwa.
Kazi yake ni kuratibu shughuli na majadiliano ya bunge. Huamua juu ya maswali ya utaratibu bungeni, ufuatano wa wabunge katika majadiliano, kutangaza matokeo ya kura bungeni na kadhalika. Ndiye mwakilishi wa bunge kwa ujumla.
[hariri] Historia
Cheo cha spika kimepatikana mara ya kwanza katika bunge la Uingereza mwaka 1377 na huyu spika wa kwanza alikuwa mkabaila Thomas Hungerford. Aliitwa "spika" (msemaji) kwa sababu kazi yake ilikuwa kutamka maazimio ya bunge mbele ya mfalme.
[hariri] Mapokeo
Kuna mapokeo mbalimbali yanayoendelezwa katika nchi zenye urithi wa mapokeo ya kisiasa ya Uingereza ingawa ni tofauti katika kila nchi mapokeo gani yaendelea au la.
Kati ya mapokeo haya ni nafasi ya spika kuwa asishikamane na upande wowote kati ya vyama vya bunge. Haya yametokea kwenye msingi wa nafasi ya spika kabla ya kuwepo kwa vyama katika historia ya Uingereza.
Alama ya spika huwa mara nyingi ni siwa ambayo ni aina ya rungu ya dhahabu inayobebwa na mtumishi wa bunge mbele ya spika akiingia bungeni. Nchi kama Uhindi, Kenya au Tanzania zimetengeneza siwa inayolingana na utamatuni wao. Siwa hutazamiwa kama kielelezo halisi cha Mamlaka ya Spika anapokuwa anatekeleza shughuli za Bunge.
Nchi kadhaa zimepokea kawaida ya kuwa spika akipenda kuchaguliwa upya hapingwi na mgombea mwingine katika jimbo lake la uchaguzi.
Katika nchi nyingi zneye cheo hiki wabunge wakihotubia bunge huelekeza matamko yote kwa spika si kwa wabunge wenzao.