Mtaguso Mkuu
Kutoka Wikipedia
Kadiri ya imani ya Kanisa Katoliki, Yesu aliwakabidhi mitume kumi na wawili uongozi wa Kanisa wakiwa kundi moja lenye mkuu wake, yaani Petro.
Vilevile waandamizi wao, yaani maaskofu wote, ni kundi moja na papa wa Roma ndiye mkuu wao. Huyo peke yake, na kundi la maaskofu likiwa pamoja naye na chini yake, ndio wenye mamlaka ya juu katika Kanisa lote.
Mamlaka hiyo inatumika kwa namna ya pekee unapofanyika mtaguso mkuu, yaani mkutano maalumu wa maaskofu uliokubaliwa na papa kuwa unawakilisha kundi hilo lote.
Kwa kiasi fulani ndiyo imani ya Waortodoksi pia, ingawa hao wanapunguza umuhimu wa mchango wa mamlaka ya papa. Kwa namna ya pekee hao wanakataa mitaguso mikuu iliyofanyika baada ya utengano uliotokea kati yao na papa. Hivyo baadhi yao wanakubali mitaguso mitatu ya kwanza tu, au ile minne ya kwanza tu, au ile saba ya kwanza tu kati ya ile 21 inayokubaliwa na Kanisa Katoliki, ambayo inaorodheshwa hapa chini.
KATIKA MILENIA YA KWANZA ILIFANYIKA MASHARIKI (UTURUKI): 1. Nisea I (mwaka 325) 2. Kostantinopoli I (381) 3. Efeso (431) 4. Kalsedonia (451) 5. Kostantinopoli II (553) 6. Kostantinopoli III (680-681) 7. Nisea II (787) 8. Kostantinopoli IV (869-870)
KATIKA MILENIA YA PILI ILIFANYIKA MAGHARIBI (ITALIA, UFARANSA, UJERUMANI): 9. Laterano I (1123) 10. Laterano II (1139) 11. Laterano III (1179) 12. Laterano IV (1215) 13. Lyon I (1245) 14. Lyon II (1274) 15. Vienne (1311-1312) 16. Kostansa (1414-1418) 17. Firenze (1439-1445) 18. Laterano V (1512-1517) 19. Trento (1545-1563) 20. Vatikano I (1869-1870) 21. Vatikano II (1962-1965)
Msimamo wa Waprotestanti ni tofauti sana, kwa kuwa hao hawatii maanani mapokeo ili wasisitize umuhimu wa Biblia. Hata hivyo wengi wao wanashikilia imani juu ya Yesu Kristo, juu ya Roho Mtakatifu na juu ya Utatu mtakatifu kama ilivyofundishwa rasmi katika mitaguso ya kwanza.
Mitaguso mikuu ya kwanza ilifanyika hasa ili kubainisha katika mafundisho yaliyogongana yapi yanalingana na imani sahihi. Mwisho wake ulikuwa kutangaza dogma fulani na kutenga na Kanisa watakaokataa kuiamini na watakaofundisha tofauti.
Kumbe mitaguso iliyofanyika baada ya farakano la mwaka 1054 kati ya Kanisa la Mashariki na la Magharibi, pamoja na kulenga umoja uliovunjika na kufundisha dogma mpya, ilishughulikia zaidi urekebisho wa Kanisa katika ngazi na nyanja zote. Kwa namna ya pekee mtaguso wa pili wa Vatikano tangu uitishwe ulijulikana kuwa wa kichungaji, yaani usio na lengo la kufundisha dogma mpya wala kulaani mafundisho mengine.