Kenya (mlima)
Kutoka Wikipedia
Mlima Kenya ndio mlima mrefu kuliko yote nchini Kenya. Mlima huu ambao hasa wenyeji waliuita Kirinyaga, una urefu wa mita 5,199. Mlima huu unatokana na volkeno iliyozimika ikikadiriwa ya kwamba mlipuko wake wa mwisho ulitokea mnamo miaka milioni 2.6 hadi 3.1 iliyopita.
Vilele vyake vya juu vinaitwa Batian (5,199 m), Nelion (5,188 m) na Lenana (4,985 m). Kuna barafuto nane mlimani lakini zinapungua kila mwaka kutokana na kupanda kwa halijoto duniani na kupungukiwa kwa usimbishaji kwa sababu ya kukatwa kwa miti mingi.