Historia ya Denmark
Kutoka Wikipedia
Yaliyomo |
[hariri] Historia ya Denmark
Utafiti wa akiolojia umeonyesha ya kwamba Denmark iliwahi kuwa na vikundi vya wavindaji tangu muda mrefu sana. Lakini katika nyakati za kupanuka kwa barafuto za Skandinavia walipaswa kundoka tena. Eneo la Denmark ilifunikwa na barafu kabisa hadi takriban miaka 13,000 hadi 15,000 iliyopita.
Tangu mwaka 4000 KK wakulima walianza kupatikana nchini. Hakuna uhakika kama Denmark ilikaliwa na Wakelti; kuna mabaki ya kiakolojia ya kuonyesha athira ya kikelti lakini haijulikani kama ni kutokana na biashara na maeneo ya Wakelti walioendelea zaidi au kama Wakelti wenyewe walikaa hapa.
[hariri] Wakimbri na Wateutonia
Watu wa kwanza waliojulikana kwa jina ni makabila ya Wakimbri na Wateutoni walioondoka Jutland katika karne ya pili KK na kutafuta nchi mpya katika kusini. Mwaka 113 KK waliingia katika eneo la Dola la Roma na Waroma waliandika habari zao. Inaonekana ya kwamba waliondoka Jutland kwa sababu ya kipindi kirefu cha baridi na njaa iliyosababishwa na mavuno mabaya.
[hariri] Waviking
Wakimbri na Wateutoni walikuwa makabila ya Kigermanik kama wakazi wote waliowafuata. Kati ya karne ya 8 hadi ya 11 BK wakazi wake waliitwa mara nyingi "Waviking" wakiogopwa na wenyeji wa Ulaya bara kwa sababu Waviking walivamia maeneo ya pwani kwa jahazi zao ndogo mara kwa mara. Lakini Waviking ni neno la kutaja watu wa Kaskazini -sio Wadenmark pekee lakini pia Waviking kutoka Norway- waliovamia na kufanya ujambazi kwenye nchi za Ulaya bara si namna jinsi watu wenyewe walivyojiita.
[hariri] Wadenmark katika Uingereza
Katika kipindi hiki vikundi kutoka Denmark walivamia hasa Uingereza mara kwa mara na kujenga makao huko. Tangu mwaka 793 walitawala eneo la Danelag (au: Danelaw) iliyoenea katika kaskazini na kaskazini-mashariki ya Uingereza wa leo. Miji muhimu katika eneo hili ilikuwa Leicester, Lincoln, Nottingham, Stamford, Derby pamoja na York. Kwenye mwisho wa kipindi hiki mfalme Knud (kiing.: Canute) alitawala Denmark pamoja na Uingereza yote hadi mwaka 1035.
[hariri] Denmark tangu karne ya kumi
Katika karne ya tisa na karne ya kumi maeneo madogo yaliunganishwa. Wafalme wa kwanza wanaojulikana kutawala Denmark yote walikuwa Garm Mzee na Harald Jino Buluu (mnamo mwaka 980 BK). Harald alikuwa mfalme wa kwanza wa kupokea Ukristo wa kikatoliki. Baada ya kifo cha Knud (tazama juu) Denmark ilipoteza maeneo yake huko Uingereza.
Mfalme Valdemar alipanusha uatwala wake kusini katika Ujerumani ya Kaskazini na kote katika Bahari ya Baltiki hadi Estonia. Wakati ule bendera ya Danebrog ilianza kutumiwa.
Katika karne ya 13 BK eneo la Denmark na nguvu ya wafalme ilipungua katika mashindano na miji ya biashara ya Ujerumani ya Kaskazini.
[hariri] Umoja wa Kalmar
Mwaka 1397 malkia Margarete I aliolewa na mfalme wa Norway. Baada ya kifo cha mumewe alitawala nchi zote mbili na baadaye pia Uswidi. Mwaka 1397 wawakilishi wa falme tatu zilikutana katika mji wa Kalmar (Uswidi ya kusini) na kuelewana juu ya "Umoja wa Kalmar" yaliyounganisha nchi zote za Skandinavia chini ya mfalme wa Denmark ilhali kila nchi iliendelea kujitawala. Wakati ule Ufini (Finland) ilikuwa chini ya Uswidi. Iceland na Visiwa vya Faroe ziliingia pia kwa sababu zilikuwa chini ya Norway wakati ule. Umoja huu uliendela hadi mwaka 1521.
Waswidi walianza kuchoka na utawala wa kidenmark wakaondoka katika umoja huu mwaka 1521 pamoja na Ufini. Lakini Norway iliendela kuwa chini ya Denmark hadi mwaka 1814.
[hariri] Tangu karne ya 16 BK
Mwaka 1537 Denmark ilijiunga na mwendo wa Matengenezo ya Kanisa na kanisa la Kiluteri likawa dini rasmi nchini. Denmark ilikuwa kati ya nchi muhimu sana ya Uluteri.
Nchi ilikuwa na mapato mazuri kutokana na kodi ya kuruhusu meli za kupita kwenye milango ya kuingia bahari ya Baltiki.
Katika vita na Uswidi maeneo ya Uswidi ya kusini yalipotelewa mwaka 1658.
[hariri] Ukoloni
Kuanzia karne ya 17 BK Denmark ilianza kutafuta koloni. Ilitawala tayari visiwa vya Greenland na Iceland kama koloni zake katika Atlantiki. Iliendelea kujiunga na biashara ya Uhindi na Amerika.
Koloni ya kwanza katika kusini ya dunia ilikuwa Trankebar katika Uhindi ya kusini mwaka 1620. Mwaka 1671 ilifuatwa na kisiwa cha St Thomas, 1718 na St John na 1733 na St Croix vyote katika eneo la visiwa vya Karibi. Denmark ilikuwa pia na maeneo madogo katika Afrika ya magharibi hasa kwa kusudi la biashara ya watumwa waliohitajika kwa ajili ya kilimo cha miwa huko Karibi.
[hariri] Karne ya 19
Wakati wa vita kati ya Napoleon na Uingereza Denmark ilijaribu kukaa nje ya mapigano. Baada ya kuwakataza Waingereza wasipite kwenye milango ya bahari ya Baltiki Uingereza ulivamia mji mkuu Kopenhagen na kuuchoma moto. Baada ya kushindwa kwa Napoleon Waingereza waliadhibu Denmark kwa kuiondoa katika utawala wa Norway iliyounganishwa na Uswidi. Lakini koloni za Greenland, Iceland, Faroe na visiwa vya Karibi zilibaki kwa nchi.
[hariri] Fitina ya Schleswig
Kuanzia katikati ya karne Denmark iliona mwendo wa utaifa uliosababisha wasiwasi kati ya wakazi wenye utamaduni wa Kidenmark na wale wa utamaduni wa Kijerumani. Mfalme wa Denmark alitawala pia majimbo ya Schleswig na Holstein.
Schleswig katika Kaskazini iliwahi kuwa jimbo chini ya mfalme wa Denmark kwa karne nyingi hata kama idadi kubwa ya wakazi walikuwa Wajerumani.
Holstein ilikuwa sehemu ya Dola la Ujerumani tangu zamani. Mkataba wa 1460 ulisema ya kwamba majimbo yote mawili hayatatenganihswa kamwe. Kama mtemi wa Holstein mfalme wa Denmark alikuwa pia na cheo ndani ya Ujerumani.
Kutokana na itikadi ya utaifa Wadenmark wengi walitazama hasa jimbo la Schleswig kama sehemu ya Denmark tu hasa kwa sababu jimbo hili lilikuwa na idadi ya wakazi wenye lugha ya Kidenmark. Wakazi walio wengi waliokuwa Wajerumani walikuwa pia na uamsho wa utaifa wa Kijerumani walikataa kuunganishwa na Denmark mbali ya kuwa na mfalme huyuhuyu. Hasa walitetea haki yao ya kuwa pamoja Holsetin.
Fitina hii ilisababisha ghasia ya Wajerumani wa Schleswig iliyosababisha vita ya 1848 - 1851 kati ya Denmark, jimbo la Schleswig na jeshi la Prussia lililosaidia Wajerumani wa Schleswig. Waingereza na Warusi waliingilia kati wakazuia kushindwa kwa Denmark. Jimbo lilibaki upande wa Denmark lakini kwa masharti ya kuendelea na hali ya pekee chini ya mfalme wa Denmark lakini si kama sehemu ya Denmark.
Mwaka 1863 Denmark ilipata katiba mpya iliyolenga kuunganisha sehemu zote za Ufalme chini ya sheria moja. Kwa katiba hii Denmark ilivunja mapatano yaliyomaliza vita ya 1848-1851. Shirikisho la Ujerumani na hasa Bismarck waziri mkuu wa Prussia walichukua nafasi hii kuanzisha vita dhidi ya Denmark iliyoshindwa na kupaswa kukubali majimbo mawili kuwa sehemu za Ujerumani.
[hariri] Karne ya 20
Denmark haikushiriki katika Vita Kuu ya Dunia ya Kwanza lakini Mkataba wa Versailles uliamua ya kwamba jimbo la Schleswig liwe na kura kama wakazi wanapendelea kukaa upande wa Ujerumani au Denmark. Wakazi wa sehemu ya Kaskazini walipendelea Denmark hivyo Jimbo la Schleswig liligawiwa.
Wakati wa Vita Kuu ya Dunia ya Pili Denmark ilivamiwa na Ujerumani mwaka 1940 baada ya mapigano ya kijeshi ya masaa mawili. Kiasili Ujerumani ilitaka hasa kutawala milango ya bahari ya Baltiki na njia ya kufika Norway iliyovamiwa na Ujerumani pia.
Hivyo utawala wa Wajerumani ulikuwa na upole mwanzoni. Serikali ya Denmark pamoja na mfalme walibaki nchini, magazeti yaliendelea kupatikana na vyama vya kisiasa vilifanya kazi. Wajerumani waliridhiki ya kwamba hawakupaswa kutumia wanajeshi wengi (waliohitajika penginepo) kuhakikisha utawala wao na ya kwamba Denmark ilisaidia uchumi wao kwa uzalishaji wa vyakula na bidhaa ya viwandani.
Tangu 1942 upinzani wa wananchi wengi dhidi ya hali ya kumilikiwa uliongezeka. Baada ya migomo mbalimbali ya wafanyakazi Ujerumani 1943 ilidai hatua kali zichukuliwe dhidi ya wafanyakazi. Serikali ilikataa ikajiuzulu. Wajerumani waliweka nchi chini ya utawala wa kijeshi.
[hariri] Ukombozi wa Wayahudi wa Denmark
Wakati huohuo serikali ya Berlin ilitaka kukamata pia Wayahudi wa Denmark ambao hadi wakati ule waliishi maisha ya kawaida - tofauti na nchi zote nyingine za Ulaya zilizokuwa chini ya utawala wa Ujerumani ambako Wayahudi walikamatwa na kupelekwa katika makambi ya KZ. Wapinzani wa siasa ya kuua Wayahudi ndani ya ubalozi wa Ujerumani huko Kopenhagen walipasha habari hii kwa siri kwa viongozi wa Denmark. Katika muda wa masaa 24 karibu Wayahudi wote wa Denmark walifichwa na wenzao Wakristo na kupelekwa Uswidi kwa maboti madogo ya wavuwi wakati wa usiku kuvukia mlango wa Oresund. Polisi ya Denmark ilikataa kukamata raia Wayahudi au kuwatafuta. Hii ni mfano wa pekee jinsi nia ya pamoja ya nchi chini ya utawala wa Kinazi iliweza kushinda mipango ya mauaji.
Kati ya jumla ya Wayahudi 8000 za Denmark 481 pekee walikamatwa. Wajerumani waliogopa kuwapeleka katika makambi ya mauti moja kwa moja kwa sababu ya hasira ya Wadenmark waliohitajika katika mipango ya uchumi wa vita. Tena siasa ya kuua Wayahudi haukutangazwa mbele ya watu - kufuatana na matangazo rasmi Wayahudi walipelekwa katika maeneo ya Mashariki ya Ulaya ili wafanye kazi. Kwa hiyo Wajerumani walipeleka Wayahudi wachache wa Denmark katika kambi la Theresienstadt huko Uceki lililokuwa kambi la maonyesho walipopelekwa wageni wa nje waliowahi kusikia habari za matendo maovu dhidi ya Wayahudi.
Kati ya Wayahudi waliokamatwa 116 waliuawa au kufa kambini. Wengine waliishi hadi mwisho wa vita.
[hariri] Denmark ya kisasa
Wakati wa vita Iceland iliamua kutangaza uhuru wake. 1948 bara baada ya vita visiwa vya Faroe vilipewa madaraka ya kujitawala lakini vilibaki ndani ya umoja na Denmark. Koloni ya Greenland ilipewa madaraka haya mwaka 1979.
Denmark ikawa kati ya nchi zilizounda UM na pia NATO. Mwaka 1973 ikajiunga na Jumuiya ya Ulaya (sasa: Umoja wa Ulaya).
Mwaka 2000 raia za Denmark walikataa kwa kura kujiunga na pesa ya Ulaya Euro.